Tuesday, January 17, 2012

Mke gani umuoe?

Utaoa mke gani, swali umeniuliza,
Awe kwako afueni, akili kukutuliza,
Atayekupa hisani, na daima kukutunza,
Nami mwana nakwambia, bila yoyote ajizi:


Oa aliyelelewea,
Hakika akaleleka,
Adabu anayejua,
Na utu kukamilika!

Oa anayemjua,
Muumba wake Rabuka,
Dini anayeijua,
Na ibada kuzishika!

Oa asiye udhia,
Rahisi wa kuchafuka,
Kinyaa anayejaa,
Ashindwe kutazamika!

Oa aliyejaliwa,
Ubongo kukamilika,
Na akili nazo kua,
Kizazi chema kutoka!

Oa asiye bandia,
Ovyo anayetumika,
Wakubwa kukusaidia,
Waezua, waezeka!

Oa aliye radhia,
Pendo aliyelishika,
Kasoro usiyemjua,
Na nuksi kuziruka!

Oa asiyesumbua,
Kwa kelele kumtaka,
Sauti anayetoa,
Hata punda kumcheka!

Oa alyemegewa,
Ya Urulaini hakika,
Wimbo anayekwimbia,
Kwa kila analotamka!

Oa sura asokuwa,
Lakini mali asaka,
Na yako inapokuwa,
Kwake iwe yatunzika!

Oa asiyekulewa,
Na tunzo akizishika,
Staha anayeijua,
Wapi pakukanyagika!

Oa asiyezitoa,
Siri zilizofichika,
Watu kuwasimulia,
Hata wasiohusika!

Oa msafi wa nia,
Uoza asiyeshika,
Marashi akijitia,
Akupandishe Mizuka!

Oa asiyejitia,
Uzungu na Uamerika,
Nguo anayezivaa,
Mapaja zisofunika!

Ila nawe watakiwa,
Katakei kutoweka,
Ni utumwa wajitia,
Kwa watumwa Amerika!

Oa asiyeonea,
Wanyonge na malaika,
Yatima anayelea,
Kama wake kutunzika!

Oa anayetambua,
Uzee utapofika,
Wazazi atawalea,
Hadi wafe waridhika!

Oa shoo asokuwa,
Majiani kujiweka,
Njiani kiguu na njia,
Kaziye kujianika!

Oa anayevumilia,
Yote yatayomfika,
Asiye na mazoea,
Ya watu kutamanika!

Oa anayeamua,
Na mipango kupangika,
Pasiwe ombwe kutua,
Nyumbani pakachafuka!

Oa anayewalea,
Wana wakaelimika,
Lukmnani kumjua,
Na yake akayashika!

Oa asiyekulia,
Wewe unapojicheka,
Oa anayekujua,
Pasiwe na kufichika!

Oa unayemuoa,
Roho na mwili kushika,
Kitu kimoya mkawa,
Yenu yote ya hakika!

Oa mwana majaliwa,
Libasi mkajishika,
Mjipambe kwa hatua,
Na kizazi kukidaka!

Oa wana wakajua,
Watu wema wazalika,
Na Mungu wakimjua,
Yao hujarehemeka!

Oa wasiotumiwa,
Na mtu au mahoka,
Ovyo wasiochezewa,
Na chama au vibaka!

Oa wasiolegea,
Ukubwa kuja ushika,
Wanaojitafutia,
Wenyewe wakajiweka!

Oa wasio balaa,
Watu watakaokucheka,
Uonekane Kinyaa,
Mchamungu wa hakika!

Oa wasio na njaa,
Lolote likakubalika,
Wajaokujiachia,
Kwako ikawa mashaka!

Oa waliotulia,
Wenye mwendo wa hakika,
Yakini wanaojua,
Haraka haina baraka!

Oa si kwa kuchagua,
Kizazi anachotoka,
Ila kwa kutambua,
Wema aliyezalika!

Oa si alichopewa,
Tajiri alozalika,
Oa kwa kutambua,
Nanyi mtatajirika!

Oa si kama sanaa,
Televisheni kutoka,
Oa yatakayofatia,
Vyema yakaandalika!

Oa hata kimyakimya,
Bila sherehe mwafaka,
Watosha kuangalia,
Kwao mliozalika!

Oa mlichochangia,
Kwa heri kikatumika,
Yatima kuwaendea,
Hali ikabadilika!

Oa kwa kunyanyua,
Mikono zije baraka,
Na sujuda kuitia,
Mmtangulze Rabuka!

No comments: