Kalamu naichukua, mazuri kukumbukia,
Baba na mama ni jaha, laiti tungelijua,
Na wakati hukimbia, twaweza kutowafaa,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Huja kutuhudumia, toka utoto tukiwa,
Ujana kutuhadaa, tuzidi kuwaegemea,
Siku zikayoyomea, na mauti kuwatwaa,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Nyumba tunapobakia, ndio tunasimulia,
Laiti tungelijua, hili tungeliwafanyia,
Ni hadithi inakuwa, maana inshapotea,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Wanangu nawaambia, vizuri haya kujua,
Dini kuizingatia, na Mola kuwajalia,
Yeye mkishamjua, wazazi watafwatia,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Lukman kajaliwa, Kurani yahadithia,
Wana alivyowalea, Mola kumshahadia,
Nyuma hawakubakia, neema walizojaliwa,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Sina cha kutarajia, ila tawhidi kuwa,
Mungu mkishamridhia, mimi yangu yatakua,
Kuomba tunatakiwa, yeye kumgeukia,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Dua zangu ninatoa, yeye kuwabarikia,
Dini kuishikilia, na kizazi kwendelea,
Musihi mwashuhudia, na kufa Islamiya,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Muogope ya dunia, na siasa za hadaa,
Moto zinazochukua, na mfukoni kutia,
Pepo itawakim bia, motoni mkabakia,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Baba na mama nalia, nimekwishaondokewa,
Wivu ninawaonea, wale waliojaliwa,
Mimi ni mwana ukiwa, machungu navumilia,
Ni nani kama mzazi, katika hii dunia ?
Tuesday, January 10, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment