Salamu hakika ua, jinsi zinavyovutia,
Kila anayetumiwa, furaha huisikia,
Mapenzi yakamvaa, kukumbukwa na jamia,
Salamu ni maua,
moyoni yanachanua,
Hupendeza watumiwa,
kama rangi za kung'aa,
Na harufu kunukia,
kama waridi radhia!
Kurani yatuambia, udugu budi kulea,
Na salamu nawambia, ni dawa inayofaa,
Jamaa wakisikia, moyoni unabakia,
Salamu ni maua,
moyoni yanachanua,
Hupendeza watumiwa,
kama rangi za kung'aa,
Na harufu kunukia,
kama waridi radhia!
Redio mkijaliwa, salamu zinatakiwa,
Nyumbani kuwatumia, hata nje walokuwa,
Intaneti hupitia, kufika hata Ulaya,
Salamu ni maua,
moyoni yanachanua,
Hupendeza watumiwa,
kama rangi za kung'aa,
Na harufu kunukia,
kama waridi radhia!
Mwanaharusi ajua, na yeye Farida pia,
Sakina namsikia, na Jamili kaelewa,
Salamu ni maua,
moyoni yanachanua,
Hupendeza watumiwa,
kama rangi za kung'aa,
Na harufu kunukia,
kama waridi radhia!
Tuesday, January 10, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment