Thursday, January 12, 2012

Uongozi ni kipaji

KAMA haukujaliwa, hutoweza kuongoa,
Hubebwa ukapakiwa, na hapo ukaishia,
Siku kukutangulia, palepale kubakia,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Siasa wanaoingia, ukubwa wanalilia,
Umeneja kwao njaa, matumbo kujijazia,
Wengine kusaidia, nahau hawajajua,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Huishi kwa kubabia, hawamanyi tasnia,
Njia wanazopitia, nchi haiwezi kukua,
Changamoto hukomaa, nao wazidi kuvia,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Uongozi kutatua, matatizo yalokuwa,
Watu wapate pumbua, maisha kujijengea,
Nchi ikaendelea, na kileleni kutua,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Uongozi ni kujua, na kuionyesha njia,
Wala sio kusifiwa, na vijambo kupambiwa,
Watu wataka nasaha, na wito kutangulia,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Uongozi mshumaa, giza kote huondoa,
Na wanaofuatia, salama kujipitia,
Pasiwe nao ukiwa, wala ya kupungukiwa,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Uongozi sio njaa, ukame nazo balaa,
Nuksi huteguliwa, njiani kuondolewa,
Pasiwe wa kuumia, kwa mipango kuandaa,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Uongozi si tamaa, vya watu kuvitumia,
Mashamba kuyachukua, usiyoyashughulikia,
Na viwanja kupangua, hata usipozaliwa,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Uongozi si kupaa, kila siku na kutua,
Budi nchi kuijua, na watu kuwaelewa,
Na kisha kuwaingia, maisha wakanyanyua,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

Uongozi si nazaa, na wongo kushupalia,
Hutakiwa kuridhia, nchi yanayoifaa,
Na chambo kuziondoa, imani zinazoua,
Uongozi ni kipaji na wala sio ukubwa!

No comments: