Thursday, January 12, 2012

Tunda na kokwa lake

Hakuna anayetwaa, kokwa akalichukua,
Wata nyama hujilia, na midomo kurambia,
Ila kwako hukataa, mbali wakalitupia,
Nyama ya tunda na kokwa, ni kipi kilicho bora.

Mshairi hushangaa, hawa wasiyoyajua,
Ubora kilichokuwa, si nyama kuitumia,
Ila kokwa kuchukua, ukapanda likazaa,
Nyama ya tunda na kokwa, ni kipi kilicho bora.

Ila katika dunia, subira wamekataa,
Hutaka cha kutumia, si cha kujitengezea,
Ukiona chaelea, kuundwa hawajajua,
Nyama ya tunda na kokwa, ni kipi kilicho bora.

Mwafrika kafubaa, mtoto bado akua,
Midoli anatupiwa, aende kuchezea,
Ni magari yalokua, na vyombo vya kutumia,
Nyama ya tunda na kokwa, ni kipi kilicho bora.

Viongozi watania, ni walaji si wa kuzaa,
Maisha wanadhania, ni kula na kutumia,
NI hesabu za kutoa, ndizo wanazozijua,
Nyama ya tunda na kokwa, ni kipi kilicho bora.

Kujumlisha hutoa, na kazi kuzidishia,
Kichekesho kimekua, kila ukiwaangalia,
Wao wazidi shupaa, nchi zazidi didimia,
Nyama ya tunda na kokwa, ni kipi kilicho bora.

No comments: