Thursday, January 12, 2012

Usitazame tu juu

Toka upate ukuu, macho chini hujatua,
Nakuasa kitukuu, utakuja kujikwaa,
Kwa kutojua mguu, ni wapi wakanyagia,
Usitazame tu juu, chini pia angalia!

Vibaya kujisahau, chini kutoangalia,
Hudondoka kama buu, pasiwe pa kushikilia,
Uonekane mafuu, kama sio mkichaa,
Usitazame tu juu, chini pia angalia!

Huyakimbia malau, chini wanaoangalia,
Jamii kuwa nahau, na methali kutumia,
Kwa kila aliye juu, chini wakamngojea,
Usitazame tu juu, chini pia angalia!

Roho ikiwa kifuu, haya hautotambua,
Majuto ni mjukuu, malalo ukisogea,
Huikumbuka juzuu, hatua mwisho ikiwa,
Usitazame tu juu, chini pia angalia!

Mwanangu acha makuu, si ya kwetu dunia,
Haipendi mabahau, wanayoing'ang'ania,
Kila kitu hudharau, na yenyewe kubakia,
Usitazame tu juu, chini pia angalia!

Milima na vichuguu, hatima huja fikia,
Na wadogo kwa wakuu, nafasi huziachia,
Na kizazi husahau, yaliyowatangulia,
Usitazame tu juu, chini pia angalia!

Walii nakaza mguu, nisije sahau njia,
Naziogopa tanuu,, balaa zinazokua,
Naitafuta nafuu, bustanini kukaa,
Usitazame tu juu, chini pia angalia!

No comments: