Thursday, January 12, 2012

Dhuluma ina kikomo

Hufika chake kikomo, dhuluma kuondolewa,
Ikaisha misukumo, adha na kusumbuliwa,
Waliomo wawe wamo, na wasiomo kupwaya,
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

Huanza na kitetemo, ubaya wa kuvizia,
Kisha kuwa mngurumo, watu ukawastua,
Kisha uwe mgugumo, panya akigugumia,
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

Dhuluma ovu mchumo, au haki kuibiwa,
Hupenda sana mfumo, siri unaochimbia,
Yawemo yasiyokuwemo, nchi ikawa yaliwa,
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

Huishi nazo ngurumo, za wongo na kutishia,
Wasiofaa huwamo, wafaao kutolewa,
Ukubwa na kilichomo, vyote uoza hutiwa,
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

Huwepo kwenye kilimo, wakulima kuibiwa,
Wakakosa msimamo, na nguvu kuwalegea,
Mwisho si kwanza kilimo, baadaye kuja kuwa,
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

Huwepo kwenye mfumo, pia demokrasia,
Mamlaka waliomo, nguvu kujiongezea,
Huwatia wasiomo, waliomo kuondoa,
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

Na viwandani huwamo, chao kujichukulia,
Angalia mtazamo, ya umma yaliyokuwa,
Wameuza kwa kichumo, nini umeambulia?
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

Kwenye biashara umo, kodi na ushuru pia,
Haki huwa ya mdomo, na sio ya kutendewa,
Ndipo huzuka migomo, wazuri kuwa wabaya,
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

Ukumbukeni msemo, penye nia pana njia,
Na sasa nawaambia, kwenye waa kuna wiwa,
Dhulumati atatwaa, motowe kwa magunia,
Dhuluma ina kikomo, Mola anapoamua!

No comments: