Thursday, January 12, 2012

Makengeza hukengua

Makengeza hukengua, ila kuona huona,
Na waliomzoea, hujua anapooona,
Konyeza hakujaliwa, macho yanavyopishana,
Makengeza hukengua, lakini sio kipofu!

Madhali anajijua, haliye hawezi kana,
Pande akiangalia, huzidisha uungwana,
Upole yake tabia, si mtu wa kubishana,
Makengeza hukengua, lakini sio kipofu!

Macho huyabinua, kama uko mbali sana,
Lakini akibambua, yasiyoonwa huona,
Mgumu kuhadithis, kwani ni msiri sana,
Makengeza hukengua, lakini sio kipofu!

Sura mwepesi kujua, macho nuru hubana,
Hata gizani akiwa, huachi kujulikana,
Imegeuka dunia, hakuna kutaniana,
Makengeza hukengua, lakini sio kipofu!

No comments: