Saturday, January 14, 2012

Umeme tunaibiwa?

Viongozi kuamua, kirahisi kuridhia,
Mashaka yananijaa, uwezo waliojaliwa,
Naona hii nazaa, uchumi tutatuua,
Umeme tunaibiwa?



Ukiritimba kuzaa, uoza uliokuwa,
Na chama kutuibia, kia kilichoingia,
Si chanzo kilichokua, hapa tulipofikia?
Umeme tunaibiwa?

Mameneja wasofa, na nchi kuajiriwa,
Mbumbumbu wa tasnia, zuzu wa teknolojia,
Kisha tunawaachia, spidi kukanyagia?
Umeme tunaibiwa?

Watumishi walojaa, tena pia wasofaa,
Shirika walipania, kama ng'ombe wa maziwa,
Kila siku kukamua, hata na damu ikiwa,
Umeme tunaibiwa?

Mijini tunalaliwa, vijijini waambaa,
Iweje asilimia, ndogo hivi ilokuwa,
Mzigo kuuchukua, na tuje kuendelea?
Umeme tunaibiwa?

Viongozi twahofia, njia wameshapotea,
VIchakani waingia, kwenye miba na balaa,
Nani wa kutuokoa, shari ikituvamia?
Umeme tunaibiwa?

Mameneja watakiwa, magwiji wa tasnia,
Watoke hata Ulaya, shirika kusimamia,
Mapfofesa wamejaa, na mafundi kwa gunia,
Umeme tunaibiwa?

Wengine waajiriwa, vibarua walokua,
Menijementi kung'aa, maamuzi kuzubaa,
Na ndugu wanaajiriwa, kwa kazi wasizojua,
Umeme tunaibiwa?

Ya babu teknolojia, ndiyo wanayotumia,
Teknohama yawia, vigumu kuielwa,
Vibovu wananunua, vyenyewe vyajiozea,
Umeme tunaibiwa?

Amerika na Ulaya, kazi zimeshapotea,
Nyumbani wanakaa, na umeme wanajua,
Ndioho walichosomea, na kulala walalia,
Umeme tunaibiwa?

Akili tungejaliwa, huko tungewafatia,
Kuzungumza kwa nia, na nchini kuwavutia,
Kwa ajira kuwatwaa, kuwekeza nako pia,
Umeme tunaibiwa?

Si Dowans kuwagawiwa, kitu wasiojipandania,
Huu uwizi twalia, nchi kwa hivi twaua,
Na wanyongaji twajua, ni nani waliokua,
Umeme tunaibiwa?

Muundo unaotumiwa, tayari umefubaa,
Shirika budi kugawa, kuwa nayo ya mkoa,
Haya ushindani kuwa, wateja kupigania,
Umeme tunaibiwa?

Ukubwa kuulilia, siyo tuliyojaliwa,
Kipaj hatukupewa, makubwa kuyajulia,
Akili zimesinyaa, ni vidogo kuvilea,
Umeme tunaibiwa?

Mifumu tumefumua, na siasa kuzitia,
Wajuzi tunawatoa, na mangimeza kutia,
Kipi kitaendelea, kuwepo wasiojua?
Umeme tunaibiwa?

OVATAIMU BALAA, NI MCHEZO UMEKUA,
KAZI YA LIMOJA SAA, SIKU NZIMA HUCHUKUA,
HAZINA YAHUJUMIWA, SISI TUNAANGALIA?
Umeme tunaibiwa?

Mikataba walotia, sisi kujadhulumiwa,
Tungali tuanwatetea, na ujanja kuutumia,
Ili kuwazawadiwa, cha mbele tulichotwaa,
Umeme tunaibiwa?

Nchi washikilia, nani atawaingia,
Hatua kuzichukua, na kuilipa fidia,
Mnyonge araruliwa, nasi tunaangalia?
Umeme tunaibiwa?

Maamuzi twagugumia, chini chini twatambaa,
Uzaini twaingia, wananchi kuwaibia,
Siasa tumepungukiwa, ni ujinga tunatumia,
Umeme tunaibiwa?

Manunuzi twaibia, na invoisi kujaa,
Upepo vilivyokuwa, ndani havitoingia,
Mdhibiti kalemaa, ndani hatojionea,
Umeme tunaibiwa?

Mnyonge budi kulia, kwa ninavyodhulumiwa,
Sina linaloingia, bila ya kuchukuliwa,
Mizigo naongezewa, hadi sasa natambaa,
Umeme tunaibiwa?

No comments: