Friday, January 13, 2012

Waungwana huungana

Waungwana lao moja, si watu wa kuumana,
Ya kwao hupanga hoja, ya wengi kuwa maana,
Akili kosa kufuja, kila ana la kunena,
Waungwana huungana, sio wanaogombana.

Huiepuka mirija, na hula wanachovuna,
Wananchi 'kuwangeleja', hilo kwao si amana,
Nao hujifunga mkaja, hali ngumu wakiiona,
Waungwana huungana, sio wanaogombana.

Na Juja na Maajuja, watawasoma kwa kina,
Huijua ngojangoja, matumbo huumizana,
Tarehe budi kutaja, na mamboye kufanana,
Waungwana huungana, sio wanaogombana.

Wanaostahili koja, afu huafikiana,
Ukubwa sio daraja, ila nafuu kuona,
Watufanyao mateja, lazima kufukuzana,
Waungwana huungana, sio wanaogombana.

Huzitamka lahaja, lugha zinapoumana,
Na watu huwa wamoja, japo wanatofautiana,
Watafute lenye tija, dunia kutulizana,
Waungwana huungana, sio wanaogombana.

Huitafuta siraja, dhiki zinapopandana,
Na mujibu utskuja, na watu wakafaana,
Mwenye shida huitaja, haja tukatimiziana,
Waungwana huungana, sio wanaogombana.

Tanganyika na Unguja, yabidi kuhimizana,
Watu wataka faraja, na sio kutafutana,
Ibakie kwenda hija, uchumi unapofana,
Waungwana huungana, sio wanaogombana.

Jina lako kulitaja, nafuu hupatikana,
Hutowakwaza waseja, yao yakawa amina,
Chimbuko lake faraja, kwako linapatikana,
Waungwana huungana, sio wanaogombana.

No comments: