Thursday, January 12, 2012

Kamasi usipotoa

Kamasi likishajaa, lazima kuliondoa,
Pua kutopulizia, huziba zikanukia,
Ukajaikosa raha, ya hewa unayopumua,
Kamasi usipotoa, pua lazima kuziba!

Kamasi usipotoa, kwa wengine ni kinyaa,
Rafiki hukukimbia, mbali nawe wakakaa,
Ukawa wawasikia, pembeni wa kuambaa,
Kamasi usipotoa, pua lazima kuziba!

Si siagi nakwambia, mkate ukapakalia,
Wengi hulinyanyapaa, hawataki jionea,
Kulificha inafaa, aibu kuikimbia,
Kamasi usipotoa, pua lazima kuziba!

Likiteremka udhia, mdomoni huingia,
Na wengine hufikia, kulilamba kwa kujua,
Litamu ninaambiwa, kwa waliolitumia,
Kamasi usipotoa, pua lazima kuziba!

Ubongo huyafagia, ziada isiyotumiwa,
Ovyo ukiyaachia, flu huweza kuua,
Usafi kuyaondoa, pua ipate pumua,
Kamasi usipotoa, pua lazima kuziba!

Chini likining'inia, puani likaelea,
Watu watakudhania, mjinga uliyepumbaa,
Waovyo huukumiwa, kwa wanaokuangalia,
Kamasi usipotoa, pua lazima kuziba!

Na ovyo kujipungia, mtu laweza mwingia,
Makusudi kudhaniwa, ugomvi ukaibua,
Pasipo kuhurumiwa, waweza kushambuliwa,
Kamasi usipotoa, pua lazima kuziba!

Kipenga nakipengua, kamasi naziondoa,
Wote wanaonijua, TAPA nilipoanzia,
Kamasi nililikataa, mwenye nalo sikukaa,
Kamasi usipotoa, pua lazima kuziba!

No comments: