Mtu usiwe mzigo, kubebwa iwe tabia,
Simama nawe kidogo, na mbele ukajongea,
Ukigeuka ni gogo, hushindwa kuchukuliwa,
Kifurushi umekua, kazi yako ni kubebwa!
Usiwe kama mdigo, chini ukang'ang'ania,
Ukadhania mhogo, ardhini wajichimbia,
Mbebaji huwa mbogo, mzigo akakataa,
Kifurushi umekua, kazi yako ni kubebwa!
Usitegemee Tigo, kuwa itakunyanyua,
Hiyo yao ni mitego, na wajinga huingia,
Vodacom si wagogo, cha bure kukupatia,
Kifurushi umekua, kazi yako ni kubebwa!
Airtel wana wigo, ziada hawatatoa,
Bila kuwa na uchago, kwanza wakajivunia,
Wakipita makorongo, ndio watakufikiria,
Kifurushi umekua, kazi yako ni kubebwa!
Zantel na usongo, lengo lao kutimia,
Vipi Hamadi wa kago, fedha akakumwagia?
Mwenyewe la njaa chango, kuna kitu kubakia,
Kifurushi umekua, kazi yako ni kubebwa!
Ndoto zako za msongo, mhemuko hukuvaa,
Usiwe kama jongoo,njiani kazi kung'aa,
Fanya yenye makanyago, msingi kujijengea,
Kifurushi umekua, kazi yako ni kubebwa!
Monday, January 9, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment