Tuesday, January 10, 2012

Utakusanya dunia ?

Mali mnazokimbilia, kujiuliza yafaa,
Mfukoni mtaitia, au ndiyo itawatia?
Hili ukishalijua, nyepesi huwa dunia,
Utakusanya dunia, au itakukusanya?

Mbio mnazokimbia, kama panya pori kua,
Wapi mtapoishia, na lipi kujivunia,
Ukuta mkifikia, wapi mtajapitia?
Utakusanya dunia, au itakukusanya?

Mnachojilimbikia, ni kipi mtachukua,
Nani mtawaachia, na vipi kujawafaa,
Au watajachochea, moto wakapulizia ?
Utakusanya dunia, au itakukusanya?

Itawakumbuka pia, mlioishi dunia,
Au mkishakufukiwa, mshaulike daria,
Kaburi kuchimbuliwa, makazi mapya kuwa?
Utakusanya dunia, au itakukusanya?

Wapi uliyoambua, akhera yatakufaa,
Mlango upi kupewa, utakapoingilia,
Nini unachotegemea, yawe yako majaliwa?
Utakusanya dunia, au itakukusanya?

Lini utarehemewa, na dua kujaombewa?
Motoni ukitupiwa, na zake zote balaa,
Au hadithi twazua, kwa kuwa sana wajua?
Utakusanya dunia, au itakukusanya?

No comments: