Sunday, January 29, 2012

Unyonyaji ukikua

BASHIRI macho hafungi, na huona kila jambo,
Msije kula mirungi, muone yasiyo tambo,
Ya mja hayamchengi, kwa sauti au wimbo,
Unyonyaji ukikua, nafuu iko njiani!

Kinyonga kwake haringi, ndiye aliyempa umbo,
Humbadili kwa rangi, adawa kukwepa mkumbo,
Na kwa mapozi ni kingi, ashinda hata mgambo,
Unyonyaji ukikua, nafuu iko njiani!

Viumbe walio wengi, ni wadogo kwa maumbo,
Na si watu wa mitungi, wala kwa wingi mapambo,
Hutafuta la msingi, mengine kwao vijambo,
Unyonyaji ukikua, nafuu iko njiani!

Lakini mlangilangi, yao yaendayo kombo,
Hutafuta kama nungwi, yaumizayo matumbo,
Kunao wavuta bangi, wajifanyao ni Rambo,
Unyonyaji ukikua, nafuu iko njiani!

Nao wenye mali nyingi, huwatumia mgambo,
Hawana chao kichungi, haki kuwa mtarimbo,
Watakayo ni shilingi, wengine kula vikumbo,
Unyonyaji ukikua, nafuu iko njiani!

Tamaa hawajivungi, hukaa nawe kitambo,
Hutumia nguvu nyingi, kuzikuza zao tambo,
Hata wenye fungu jingi, huzama kwenye mkumbo,
Unyonyaji ukikua, nafuu iko njiani!

Omwami na kina mangi, wanayaguna mafumbo,
Kadhalika na wasangi, na watani zao Rombo,
Hukiondoa kigungi, hata wakenda Urambo,
Unyonyaji ukikua, nafuu iko njiani!

Mwana muulize Dingi, kama naye ana jambo,
Nawe uwe ni mchungi, kunusuru lako tumbo,
Na ukaushe matangi, kwa dhuluma yake chambo,
Unyonyaji ukikua, nafuu iko njiani!


Januari 29, 2012
Dar es Salaam

No comments: