Sunday, January 29, 2012

Urithi ulio bora

Ukirithisa ukweli, watoto watajaliwa,
Kalitangaza Jalali, jaza anayeitoa,
Iwapo chako halali, neema hukujalia,
Urithi ulio bora, ni ukweli kurithisha!

Imani ukitawakali, Manani hukwangalia,
Hakika huwa aali, mazuri kukujalia,
Huepusha idhilali, salama nyumba ikawa,
Urithi ulio bora, ni imani kurithisha!

Busara kuinakili, vizazi hujavifaa,
Jamii kuifadhili, ikawa yasaidia,
Wote wasio akili, uchi waje kubakia,
Urithi ulio bora, ni busara kurithisha!

Hekima si kitu ghali, ila wachache hupewa,
Wengi wasio akili, wavivu kuitumia,
Wengine ni mabahili, uchoyo huwazuia,
Urithi ulio bora, ni hekima kurithisha!

Hukamilika jamili, hisani ukitoa,
Wanyonge kuwafadhili, afueni wakajua,
Ukiwa mkavu wali, bado husherehekea,
Urithi ulio bora, ni hisani kurithisha!

Wema ni yetu asili, viumbe tumeumbiwa,
Ilal shetani katili, moyoni hutupindua,
Tukafanya ujahili, na njia kuipotea,
Urithi ulio bora, ni mazuri kurithisha!

Huiambaa adili, katika hii dunia,
Mabaya tusikabili, na mazuri kuambaa,
Hukasirika Jalali, na adhabu kuitoa,
Urithi ulio bora, ni adili kurithisha!

Ukoo uso asili, kabila hulikimbia,
Huipoteza fasili, ikaisha historia,
Wakabaki ni kalili, ya kwao wasiyojua,
Urithi ulio bora, kuenzi utamaduni!

Nchi isiyo asili, msingi hujapotea,
Kadhalika mihimili, kusimama kufulia,
Ikaanguka kikweli, pasiwe wa kuinyanyua,
Urithi ulio bora, kuenzi yetu asili!

Mama wa yetu asili, Kiswahili kutambua,
Bila kukipa akili, tutageuka vichaa,
Tushindwe kuukabili, utandawazi wa dunia,
Urithi ulio bora, kuienzi lugha yetu !

Kufunzia Kiswahili, ndio tutaendelea,
Itazame Brazili, China na India pia,
Ni wasio na akili, ndio wasiolijua,

Maovu kwa Kiswahili, watu wanayalewa,
Desturi na asili, hapa tukichanganyia,
Rijali na wanawali, viumbe kamili huwa,
Urithi ulio bora, ni maovu kuepusha!

Januari 29, 2012
Dar es Salaam

No comments: