Tuesday, January 24, 2012

Utoto mtihani

Kuna watu wasokuwa, hata umri ukiwa,
Utotoni hubakia, utu uzima kupwaya,
Na wanayojifanyia, tazama utawajua,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Utoto unapoanzia, hukua na kukomaa,
Na siku ikifikiya, ya utoto huachia,
Ila ukiendeleya, vingine hukudhania,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Mtu mzima kulia, kubwa jinga tutajua,
Na mwanamme ukiwa, tena ni kubwa balaa,
Hulia bila kulia, chinichini kugumia,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Ovyo kutembeatembea, bila nalo lengo kuwa,
Jambo haujaazimia, wala shabaha kutiya,
Ukifika unakaa, hata usipotakiwa,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Midoli kuichezea, ukubwani haijawa,
Ila ukiendeleya, kasoro tutakutia,
Ukubwani hujaingia, bila haya kuachia,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Wanasesere nunua, watoto kuwagawiya,
Ila ukiwachezeya, tuhuma itaingiya,
Majinuni hudhaniwa, watu kukukimbiya,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Ukubwa ukiingia, vipo pia vyenye unaa,
Ni vitu navyo vifaa, wote tunavyovitumia,
Mmoja akizidishia, utoto hulalamikiwa,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Utoto nyingi tamaa, vitu kuvikimbilia,
Hata hatari vikiwa, hadi ajali ikawa,
Wazazi wawe walia, nuksi kujawavaa,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Ukubwa huutambua, uiyonapo kinaya,
Mtu kutochanganyikiwa, na lolote linalokuwa,
Ajua pa kutulia, na wakati kutumia,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

Hakubali kudanganywa, kama mtoto akiwa,
Na aliye muelewa, hadanganyi wengine pia,
Ukubwa kuzingatia, ukweli kutochezea,
Utoto nao mtihani, kuna watu wengi sana,
kabisa wasiokuwa !

No comments: