Thursday, January 12, 2012

Weusi sio nuksi

Weusi kwetu nemsi, wala hauna ubaya,
Katuchagua Qudusi, yaliyo bora maua,
Bustani mahsusi, kusia kwenye dunia,
Weusi sio nuksi, nuksi ni roho mbaya.

Vingine anayehisi, moyoni amekosea,
Aambaa ibilisi, imani tulivyojaa,
Waliokuwa damisi, walishawahi sikia,
Weusi sio nuksi, nuksi ni roho mbaya.

Amejaa wasiwasi, Afrika ahofia,
Inasemwa ibilisi, ndio tutakaomfaa,
Akawa hana nafasi, dunia akaikimbia,
Weusi sio nuksi, nuksi ni roho mbaya.

Weupe wanaasisi, sisi twahitimishia,
Inawadia nakisi, tutachukua dunia,
Kwa akili na nafasi, wengine nyuma wakawa,
Weusi sio nuksi, nuksi ni roho mbaya.

Wetu mkubwa mkosi, wazungu kutegemea,
Tukiacha hii nuksi, huru kweli kuja kuwa,
Kuna yaliyo fususi, Mola atatujalia,
Weusi sio nuksi, nuksi ni roho mbaya.

Magharibi ni nuksi, oneni tulikoanzia,
Na sasa ni fahirisi, Mashariki yaingia,
Tukiwadaka kisusi, uchumi hauachi kua,
Weusi sio nuksi, nuksi ni roho mbaya.

Ukubwa wenye nafasi, wa vitu kujiundia,
Kisha zetu almasi, ghali kujiuzia,
Na dhahabu kuakisi, wenyewe kujichimbia,
Weusi sio nuksi, nuksi ni roho mbaya.

Mafuta yakidurusi, wengine kutoachia,
Mshirika wa Urussi na China kuwatumia,
Walio nayo nuksi, mbali kuwaambaa,
Weusi sio nuksi, nuksi ni roho mbaya.

No comments: