Maamuzi ya hasira, watu yasoangalia,
Ubabe unaofura, hadi ukajimwagia,
Si akili kutumia, ni ujinga imekua,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa.
Watoto kuwadhania, vijana waliokuwa,
Madai mwayakataa, bila kuzungumzia,
Vyombo vyao mwavamia, mamluki kuwekea,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa.
Jeshi mnalitumia, kwa upuuzi yalokua,
Gharama kuzitumia, badala ya kujijengea,
Vingine hujadhaniwa, na tuhumu kuwekewa,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa.
Udikteta mwatumia, na si demokrasia,
Mengi mwajiharibia, kwa kidogo kilokuwa,
Mbele hamwezi wazia, mwawaza ya domo na pua,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa.
Wagonjwa wanaumia, na wengine kujifia,
Kisa mmeyachukia, kweli mnayoambiwa,
Hekima inapotea, na busara mwachimbia,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa.
Nchi yataka ulua, na wala sio kujua,
Matatizo kutatua, na sio kuyakimbia,
Kujenga na kupaua ndio kazi si kuezua,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa.
Watu wataka kukua, na sio kudidimia,
Maisha ni kuokoa, na sio kuteketea,
Na shida kuziondoa, si mtu kusingizia,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa
Sheria mwazipindua, kisha zinawapindua,
Wapi huru mgombea, Hamadi huru akawa,
Mwalia wanasheria, na makosa mwayajua?
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa
Gharama mwatuongezea, mfumuko unakua,
Hayawezi kutokea, mnayotuhadithia,
Mfumuko kupungua, na nchi kuendelea,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa
Twataka fikra mpya, za zamani zasinyaa,
Wajuaji kupangua, tuwe na wasiojua,
Wajisomeshe kwa nia, matatizo kuyajua,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa
Yameoza mazoea, na sheria zafubaa,
Minyororo imekua, ustawi yazuia,
Busara wasiokuwa, wazidi kung'ang'ania,
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa
Viatu twashindwa vaa, ukubwa vyatuzidia,
Utoto tunarudia, udongo kuuchezea,
Wakubwa watushangaa, niani kinachotokea?
Maamuzi mengineyo, ni nusu ya ukichaa
Tuesday, January 10, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment