Monday, January 9, 2012

Pamwe na maringo yote

MWANADAMU hukalia, inayoitwa dunia,
Juu yake kutembea, na mengi kujifanyia,
Ila siku huwadia, dunia kumfukia,
Pamwe na maringo yote, ni chakula cha udongo.

Uhai akiupewa, nafusihuifutua,
Akajiona kakua, na mengi kujidhania,
Vingi kuvifikiria, ni chini vilivyokua,
Pamwe na maringo yote, ni chakula cha udongo.

Na dini wasiojua, kubaya huelekea,
Wakubwa kujidhania, na maguvu kutumia,
Mali yote kujitia, ndio wamejichumia,
Pamwe na maringo yote, ni chakula cha udongo.

Yafaayo huachia, wakashika ya hadaa,
Njia huchanganyikiwa, hatimaye kupotea,
Wakaiacha dunia, bila kitu kuchukua,
Pamwe na maringo yote, ni chakula cha udongo.

Mengi hujilimbikia, hata wasivyotumia,
Na siku ikiwadia, vyote wataviachia,
Wahuni wakatumia, madhambi kumwongezea,
Pamwe na maringo yote, ni chakula cha udongo.

Kukumbusha inafaa, ni wajibu twaambia,
Pengine huja sikia, hata wachache wakiwa,
Nao wakajiokoa, na peponi kuingia,
Pamwe na maringo yote, ni chakula cha udongo.

No comments: