Sunday, January 8, 2012

Ni sanda na sio suti

Unayaona umati, mengi yasiyo ya dhati,
Na kwazo mita na futi, vipimo wanadhibiti,
Waipate ithibati, isiyo na usaliti,
Ndio huu uamsho,
ya kwetu ni tofauti:
Na nguo yetu ya mwisho,
ni sanda na sio suti !

Wanaokimbia shoti, kwa nafsi na baiti,
Wakauata umati, wazidi kushuka chati,
Awaona Muqliti, na kwake hawa hayati,
Ndio huu uamsho,
ya kwetu ni tofauti:
Na nguo yetu ya mwisho,
ni sanda na sio suti !

Sijui mwisho ubeti, na nukta siiwati,
Njia sio katikati, hayo yanakosa dhati,
Picha watu hawapati, na bishara haileti,
Ndio huu uamsho,
ya kwetu ni tofauti:
Na nguo yetu ya mwisho,
ni sanda na sio suti !

Maisha ni mkakati, na kufanza utafiti,
Ngome si ya moja geti, njia nyingi ni shuruti,
Na akili mahluti, haziachi kudhibiti,
Ndio huu uamsho,
ya kwetu ni tofauti:
Na nguo yetu ya mwisho,
ni sanda na sio suti !

Lawama hazifukuti, wala kuling'oa bati,
Ustawi si bahati, ni kunuia kwa dhati,
Mabadiliko huleti, bila ya kujizatiti,
Ndio huu uamsho,
ya kwetu ni tofauti:
Na nguo yetu ya mwisho,
ni sanda na sio suti !

Kamati kubwa kabati, au sefu na dawati,
Utakayo huyapati, hupata yaso garanti,
Fikra sio mashuti, ni nyavu kama si neti,
Ndio huu uamsho,
ya kwetu ni tofauti:
Na nguo yetu ya mwisho,
ni sanda na sio suti !

Waogao hawatoti, ila kwa wenye makoti,
Vipande hivi si doti, na miaka haitokoti,
Wakati hatuukuti, hata kwa ndege na jeti,
Ndio huu uamsho,
ya kwetu ni tofauti:
Na nguo yetu ya mwisho,
ni sanda na sio suti !

Kiwasheni kibiriti, nuru iwake katiti,
Na moto ukidhibiti, mwanga usitusaliti,
Maisha si kismati, ila ni kujizatiti,
Ndio huu uamsho,
ya kwetu ni tofauti:
Na nguo yetu ya mwisho,
ni sanda na sio suti !

No comments: