Tuesday, January 17, 2012

Nchi ya wanasesere

KATIKA hii dunia, ya wajinga wasojua,
Ya vijinga kujifia, moto visivyochukua,
Ni rahisi kutambua, kwanini tunadidimia,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Watu waliolemaa, wasoweza jisomea,
Akili wasiojua, jinsi ya kuzitumia,
Ujinga wanaooa, kisha nao wakazaa,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Na wanaotegemea, ya mzungu kuwafaa,
Walokufa kuvumbua, wakabaki kuchimbiwa,
Huna la kutarajia, ila kuja kufukiwa,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Pipo wanaoogaiwa, vito wakaviachia,
Shanga wanaopokea, almasi wakatoa,
Na mitumba kuchukua, dhahabu wakaachia,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Watu waliojaliwa, bila wao kujijua,
Kwingine wanaohemea, badala chao kutwaa,
Chao wasichojivunia, ila kukishindilia,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Wavunao na kutoa, wengine kwenda tumia,
Migumba isiyozaa, wao kinachowafaa,
Huwezi acha kulia, jinsi wasivyojijua,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Misingi wasiojua, wapi pa kusimamia,
Nasibu kukadiria, hakika lililokuwa,
Neema wanayoua, na nuksi kuzivaa,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Railimali zavia, kwa motisha kupumbaa,
Chao wasichoringia, na ghali kukusudia,
Na ndani wanaojua, ndiko kuanza pafaa,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Nchi ya wafao njaa, hali ardhi imejaa,
Ilo asili mbolea, na rutuba ya kumea,
Hila zinazowaumbua, na mikenge kuingia,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Watu wasiovumbua, kazi yao kwagizia,
Vijavyo wasobagua, takataka zikajaa,
Wapendao jisifia, kwa sifa za kununua,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Nchi ninayoililia, macho bure kuyatoa,
Watu wasiosikia, huku wadhani wajua,
Ufu wanaoupokea, hali hai wamekua,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

MIzani huzitumia, zilizokwishakataliwa,
Na sheria zenye njaa, uporo zinazopewa,
Mambo hayana kikoa, na udugu hautokuwa,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Hila wanaotumia, ya kwao kujipatia,
Vya wengi wanaoua, vya kwao kujichumia,
Akhera wasiojua, na laana wallilia,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Kizazi chao huua, kabla hakijazaliwa,
Kwa laana kulaniwa, matumboni kuingia,
Heri kujawakimbia, yatima wanapokua,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Ni wanasesere wawa, vingine haitakuwa,
Yanatisha majaliwa, kwao yatakayokuwa,
Toba tusipoitoa, na kuisahihisha njia,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

Rabana nakulilia, mchana uliokuwa,
Na usiku nao pia, hadi utaponisikia,
Nchi yangu Tanzania, upate kuiongoa,
Nchi ya wanasesere, daima huchezwa shere!

No comments: