Thursday, January 12, 2012

Pua ikishafariki

Pua ikishafariki, marashi haisikii!
Hata uchome mshikaki, kitu haitotambua,
Utakula kisibaki, pasiwe anayejua,
Pua ikishafariki, harufu haisikii,

Haijawa mamluki, nani ataitumia,
Viozavyo si laiki, na vyenye ladha si riha,
Maisha haidiriki, mengineyo kujua,
Pua ikishafariki, marashi haisikii!

Hainayo uzandiki, ajali huvumilia,
Ila sura itabaki, taswira kusaidia,
Iwe yenye mantiki, usoni ikatulia,
Pua ikishafariki, marashi haisikii!

Ila haiwi mshiriki, kwa isyoyaelewa,
Nyuma itatabaraki, mbele haitotangulia,
Ikasahau ashiki, na kawaida kujua,
Pua ikishafariki, marashi haisikii!

Haiwezi jidhihaki, marashi kuyatumia,
Ila kama yahakiki, wengine kuyasikia,
Yenyewe haiafiki, kuvaa isichokivua,
Pua ikishafariki, marashi haisikii!

No comments: