Sunday, January 8, 2012

Kizungumkuti

Chaja kizungumkuti, mageuzi ni shuruti,
Hili kama hatufati,maisha ni hatihati,
Katu hatufurukuti, hujazaliwa wana njiti,
Kizungumkuti chaja, mabadiliko shuruti!

Nchi kama haiteti, ni kimya cha mauti,
Milipuko huzatiti,katikati ya umati,
Huyapoteza mabati, nyumba zikawa za makuti,
Kizungumkuti chaja, mabadiliko shuruti!

Haziishi tashtiti, na thawabu hupukuti,
Huisha piga magoti, kiburi kikisaliti,
Na amani hauleti, kwa kuwa mtanashati,
Kizungumkuti chaja, mabadiliko shuruti!

Yameisha maliwati, akili zangu katiti,
Ngoja nilivae koti, sebuleni nikaketi,
Wakati huu sikuti, wajukuu wataketi,
Kizungumkuti chaja, mabadiliko shuruti!

Sintoiazima doti, kwenye nyumba ya makuti,
Kadhalika nayo suti, labda kama sivuti,
Na hasara siipati, kwa haya nikiwa smati,
Kizungumkuti chaja, mabadiliko shuruti!

No comments: