Thursday, January 12, 2012

Mbwa uliyemtuma

Mbwa uliyemtuma, akili amejaliwa,
Kasita watu kuuma, wewe anakushangaa,
Auliza umemtuma, panapostahilia?
Mbwa uliyemtuma, amekataa kuuma!

Mbwa ameshasimama, bwana anakuangalia,
Ataka kurudi nyuma, njia ameikosea,
Wamfanzia zahama, huhofu kukurukia?
Mbwa uliyemtuma, amekataa kuuma!

Mambo leo si salama, mbwa watu asikia,
Tena anayo hekima, haachi kufikiria,
Na bwana unayemtuma, aweza kukugeukia,
Mbwa uliyemtuma, amekataa kuuma!

Hataki dhambi kuchumba, haki anang'ang'ania,
Hata vipi ukimsema, huwezi kumtumia,
Tajiri una lazima, mkakati kuvumbua,
Mbwa uliyemtuma, amekataa kuuma!

No comments: