Saturday, January 14, 2012

Wacha wale raha

Wacha wale raha leo, kesho watalia sana,
Maisha kama mgao, na watu hupokezana,
Ni wachache wajuao, neema zisizosana,
Wacha wale raha ndogo, kesho watakonda sana !

Hadithi na mapokeo, haya yameona sana,
Na dunia kama chuo, weledi si wengi sana,
Na mambo yawapitayo, huja mwishoni kuona,
Wacha wale raha ndogo, kesho watakonda sana !

Wa Pwani kwenye mwambao, bahari husema sana,
Kungwi na wawaleao, kwao yanajulikana,
Na vyungu wainjikao, sio hao wabebao,
Wacha wale raha ndogo, kesho watakonda sana !

Mambo yataka tambuo, utotoni na ujana,
Wazazi waelewao, haya huwafunza wana,
Wasio wakati nao, hubaki wakapishana,
Wacha wale raha ndogo, kesho watakonda sana !

Na watenzi wajuao, tungo zao za maana,
Husema maneno hayo, na kuandika kwa kina,
Ila ni wajaliwao, huweza kuja yaona,
Wacha wale raha ndogo, kesho watakonda sana !

No comments: