Thursday, January 12, 2012

Huwezi amuru pepo

PEPO zimeshaafiki, kwenda zinakokutaka,
Vipi wewe mnafiki, kuzizuia wataka,
Silaha yako mkuki, Uatlasi wautaka?
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Pepo hazibabaiki, njia zikisha ishika,
Hutokea Uturuki, hadi makwetu kufika,
Tena bila ya hamaki, pasipo kuserereka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Ila hupuliza chuki, Mola anapokasrika,
Kufanya kubwa mikiki, mpaka hadi mpaka,
Na mtu hasalimiki, Ila Mola anayetaka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Ni kipi unamiliki, uwezo ukaamka,
Wewe ni mtu wa dhiki, hili halijageuka,
Maumbile hujinaki, yamekuwa wako paka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Na pepo hazitishiki, hata ungeliibuka,
Uanze kuzidhihaki, kwa nguvu unazitaka,
Ziende zikahamaki, wewe unakokutaka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Mtawala mashariki, kaipa hii hakika,
Na haachi kuzilaki, kwa kila zinaposhuka,
Na kuziuliza haki, kama hazijaipituka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Na wewe mwanakindaki, ukubwa unautaka?
Himaya yako mswaki, na maji kata kutweka,
Ni ng'ombe na mshikaki, hadhi yako yafahamika,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Ndoto zako zitaliki, au utaathirika,
Ulo nacho kisibaki, malaika kukupoka,
Uwe haueleweki, kwa kila unalotamka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Ramani nimeicheki, safariyamalizika,
Ila kuna mahandaki, njiani wameyaweka,
Vizuri kutahamaki, yasije yakalipuka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Ungeacha kuhamaki, na uumba kujiweka,
Ingekuwa ni riziki, leo yanayoponyoka,
Sasa umeshajidhiki, ungeanza kunyanyuka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Umri wake hufiki, atomu hautojitwika,
Upepo unadiriki, kwa milioni miaka,
Na wewe hauna chuki, watimiza ya Rabuka,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

Hauna ustahiki, hautaki madaraka,
Ila nguvuze za haki, hakuna lisilofanyika,
Na hata ukidiriki, mwenywe utajizika,
Huwezi amuru pepo, huenda zinakotaka!

No comments: