Thursday, January 12, 2012

Nywele zilizojikunja

Napaswa haya kujua, wanangu kuwaambia,
Nini kilichotokea, hadi fakiri tukawa,
Haya tumejitakia, au sisi twaonewa?
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Nini kilichopungua, hapa kwetu Tanzania,
Ardhi tumejaliwa, rutuba iliyojaa,
Na madini yametiwa, ndani yanaelemea,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Mito kote hutambaa, na maziwa yamejaa,
Visima twajichimbia, na chemchemi hukua,
Lakini twalia njaa, kila tukiamkia,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Akili hatukupewa, makapi tunatumia?
Au tumehujumiwa, zezeta tumeshakua?
Wengine watutumia, na hatwezi jihudumia,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Urefu hatukupewa, kcihwani tukajaliwa,
Tulichokiambulia, wa chini uliokua,
Jumlisha na kutoa, sifuri inabakia,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Shuleni tukipitia, sifa tunazichukua,
Kazini tukiingia, utoto tunarudia,
Hatuna la kuvumbua, wala jipya kuzua,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Kinyaa tumeshakua, hata kwa tuliowazaa,
Hawaeshi kuulizia, nini kinachoendelea?
Kimya chawasumbua, maiti watudhania,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Sifa twajipalilia, vya ushuzi vilokua,
Na vichwa kutanua, hata kwa tusiojua,
Kisirani tumekua, ukubwa watuzuzua,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Ulaya tukiingia, vipofu tunabakia,
Hatuoni cha kufaa, nchi kuja iinua,
Twabaki twashangaa, majuha tunabakia,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

Ndio kisa kuulizia, tutafute kujijua,
Kwani tusipojijua, katu hatutaendelea,
Fakiri tutabakia, watumwa wa majaliwa,
Nywele zilizojikunja, eti fikraze finyu?

No comments: