Friday, January 13, 2012

Viongozi magumashi

Viongozi magumashi, ni wazuri kwa nakshi,
Ila siwajumlishi,kwenye bora matamshi,
Kazi yao ushawishi, japo nyama washiwashi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Wapendeza kwa ucheshi, ila hawana upishi,
Wapikacho matapishi, na hili sio uzushi,
Husema hawapandishi, lakini hawateremshi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Ni wazuri matoashi, na nafasi haitoshi,
Ila sio waanzilshi, kwa yenye utamanishi,
Kawaida ni wabishi,na makisha hawashushi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Daima walazimishi, na kisha walalamishi,
Fikra zao kijeshi, kukokota wasoishi,
Na ya kwao madishi, ya umma hayaonyeshi,
Nitabakia mshashi kwa kazi ya pushipushi!

Kushushua ni watashi, na kuzomea uashi,
Wakkipewa bakshishi, kila kitu ni ucheshi,
Hawanuni kwa tapishi, kwao ulaji na nyweeshi,
Nitabakia mshashi kwa kazi ya pushipushi!

Vigelegele wazushi, hata palipo mazishi,
Ni mizigo huishushi, wakubwa hawabakishi,
Ni mswaki na burashi, ndipo menu huwa freshi,
Nitabakia mshashi kwa kazi ya pushipushi!

Mengi ni mafurushi, ndani kitu hakiishi,
Ni garasha na mijeshi, hutembea na beleshi,
Na yao hayenda joshi, kwani sio waendeshi,
Nitabakia mshashi kwa kazi ya pushipushi!

Wengine hawaharishi, kinyesi bali matusi,
Tabia yao uzushi, daima hawana utashi,
Huishi kama waishi, kumbe ya watu madishi,
Nitabakia mshashi kwa kazi ya pushipushi!

Huona ya wote poshi, na mengine hatarishi,
Wa Mtwara hadi Moshi, wajua wanavyoishi,
Ulaya hapawatoshi, kwa milo na bakshishi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Hali kwetu ni mazishi, na matatizo hayeshi,
Haviishi vifurushi, vya zawadi na mapishi,
Hugongana matarishi, ajabu hawaangushi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Watu hutaka kuishi, na kuwa kama arshi,
Ukubwa hauzeeshi, neema virutubishi,
Hili halina ubishi, shaibu bado waishi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Hamsini haitoshi, maisha tunayoishi,
Huyakwepa mazamishi, na kuchelewesha mazishi,
Hili hawababaishi, wamejaa magumashi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Wanaosha hawaoshwi, hawajui matamshi,
Ni harusi si mazishi, mengine waweza gushi,
Wekeza yao uashi, na kutuma waandishi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Tarafu haiwachoshi, hugeuzwa king'arishi,
Wana walio wabishi, watakao wasiishi,
Huishia na hashishi, madawa navyo vimoshi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

Refu sana garimoshi, ila kungoja hukeshi,
Hayazeeki marashi, ila kwenye matapishi,
Naishi kama siishi, ila hawanitamanishi,
Nitabakia mshashi, kwa kazi ya pushipushi!

No comments: