Tuesday, January 17, 2012

Itihari

ITA wanaokusifu, kilemba ukashonewa,
Uongo watakwambia:
Yumkini huamua, uongo ukitumia,
Dhihaka wakadhania, raia waliokuwa,
Na heshima hufifia, na utu ukapungua.

ITA wanaokusifu, kilemba ukashonewa,
Mazuri watakwambia:
Watayaficha mabaya, usipate kuyajua,
Rangi nje huipakaa, hali ndani kumevia,
Uoza huufukia, marashi wakayatia.

ITA wanaokusifu, kilemba ukashonewa,
Hadithi wataitoa:
Ndefu isiyotulia, na sababu kukwambia,
Na kisha utaamua, kwa uliyosimuliwa,
Abunuwasi ukawa, kila wakikusikiya.

ITA wanaokusifu, kilemba ukashonewa,
Halali watakwambia:
Ufalme umepewa, unaweza kuamua,
Hata mabaya yakiwa, ni budi kuitikiwa,
Dhalimu utaishia, kizazi kikalaaniwa!

ITA wakuzomeao, ya kwao ukasikia,
Ukweli wakakwambia:
Utaweza kuamua, ukweli unaujua,
Ukichemsha twajua, haukuwa nayo nia,
Kila mtu majaliwa, hupewa alojaliwa.

ITA wakuzomeao, ya kwao ukasikia,
Uongo hawatafukia:
Haki watazingatia, na ukweli kukwambia,
Msimamo kubakia, ushahidi kujapewa,
Na utakaloamua, Mola budi nawe kuwa!


ITA wakuzomeao, ya kwao ukasikia,
Mbaya watakutajia:
Unaowategemea, kichinichini hubwia,
Yao wakajifanyia, sio uliyoyaamua,
Haya hujawaumbua, wenyewe kujiondoa!


ITA wakuzomeao, ya kwao ukasikia,
Dhuluma huikataa:
Na mnyonge huridhia, hukumu utayotoa,
Haki ikikutangulia, hauwezi kupotea,
Na hapo ndipo hukaa, Mola anayesifiwa!

No comments: