Saturday, January 21, 2012

Kawa lisipokuwepo

Kawa ninakuulizia, wapi umepotelea,
Mambo kwa leo balaa, waziwazi vyabakia,
Hata vinavyotakiwa, watu kutokuvijua,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

Kila kitu wazi huwa, toka kawa kupotea,
Dhahiri vyote hujua, hata siri vya kutiwa,
Ni sinema ilokua, watu wanajionea,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

Mama nilivyomjua, kawa alilitumia,
Watoto hatukujua, baba tukimpelekea,
Hadi akalifunua, nasi tukaruhusiwa,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

Sasa vyabebwa huria, njenje vimekuwa,
Aina unaijua, na ukubwa kukadiria,
Na rangi utazijua, zote zilizonakshiwa,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

Siyaoni maridhia, haya yanayotokea,
Ninaona ni udhia, na raha inapotea,
Wazee nawalilia, mila hii kurudia,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

Uswahili majaliwa, desturi maashallaa,
Uzungu twakimbilia, hadi nguo kujivua?
Hakika nawashangaa, viumbe mliokuwa,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

Utamu unapungua, kila kinachovuliwa,
Ndio maana zajaa, ndoa zinazojifia,
Yakizidi mazoea, haraka huwa udhia,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

Watu wanaililia, sapraizi mwajua,
Wazungu waliokuwa, ni mila imeenea,
Mojawapo ndilo kawa, tunapaswa kutumia,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

Maneno nawaambia, kazi ni kufikiria,
Mazuri mkiyajua mtayashughulikia,
Likajarejea kawa, kama tulivyoanzia,
Lisipokuwepo KAWA, kila kitu njenje!

No comments: