Friday, January 27, 2012

Uongozi si tamaa

Ukubwa wanaolilia, na juu kunyanyuliwa,
Inafaa wakajua, uongozi si hidaya,
Zawadi unaokuwa, kubaya utaishia,
Uongozi si kutaka, bali uwezo wa mtu!

Uongozi haijawa, na wala haitakuwa,
Mtu akateuliwa, na usukani kutwaa,
Lazima kuchaguliwa, ikawa wakubaliwa,
Uongozi si kupenda, bali kipaji cha mtu!

Uongozi si kung'aa, kwa rangi nje ukawa,
Na harufu kunukia, Uswizi zikitokea,
Wala sio matambaa, hata aghali yakiwa,
Uongozi si ukubwa, bali unachokifanya!

Uongozi sio njia, mtu kujineemeshea,
Huo ni ulafi huwa, mama yake ni tamaa,
Na uroho kuzidia, vitu kujilimbikia,
Uuongozi sio cheo, ila kukidhi matakwa!

Uongozi sio njaa, kwenda iganga ikawa,
Kila kitu kuchukua, hata akiba za wakiwa,
Wala si tumbo kujaa, kwa halali visivyokuwa,
Uongozi sio posho, bali watu kuwafaa!

Uongozi si nazaa, wengine kuwafagia,
Pembeni wao wakawa, ukaachiwa yote njia,
Hilo twaita balaa, na riha isiyofaa,
Uongozi si ving'ora, bali ni unyenyekevu!

Uongozi si kupewa, mamlaka kuchukua,
Ukubwa kujimegea, faida usiokuwa,
Na watu kuwaonea, hata usiowajua,
Uongozi si kutaka, bali uwezo wa mtu!

Ukubwa sio tamaa, kupenda kitu ikawa,
Huo ugonjwa wa ndaa, hukataliwa na ndia,
Kichwa huwa ni mkia, na mkia kichwa ikawa,
Uongozi si kupenda, bali kipaji cha mtu!

Uongozi si hisia, kitu kutozingatia,
Ikawa wa kutumia, kutafuta kutojua,
Uongozi hutanzua, matatizo kuondoa,
Uongozi si ukubwa, bali unachokifanya!

Uongozi hutambua, njia za kuendelea,
Sio kutoendelea, kisha ukajisifia,
Hata majuha wajua, hili hutowatania,
Uuongozi sio cheo, ila kukidhi matakwa!

Uongozi mashalaa, mkweli hatolilia,
Wenyewe utamjia, mtu alochagulia,
Chini kunyanyuliwa, juu akajajaliwa,
Uongozi sio posho, bali watu kuwafaa!

Uongozi si kupaa, bali kuyapalilia,
Taratibu kuingia, na juu kujipndia,
Mida ikishaingia, hodi utazisikia,
Uongozi si kunena, bali ni kujiandaa!

Uongozi si kupewa ubwabwa ukapokea,
Kwenye sahani kutiwa, uanze kujimegea,
Mwenyewe kuupakua, balaa huziondoa,
Uongozi si udenda, ni mbegu kujipandia!

Uongozi haujawa, nasibu kunasibia,
Kadiri inatakiwa, watu wakakufatia,
Nyumayo wakishakua, ndio vitani kwingia,
Uongozi si bahati, ni kadiri kuikuza!

Uongozi haujawa, wafuasi bila kuwa,
Au wanaokuchezaa, kama si kukupindua,
Jingine wasofikiria, ila urithi kuutwaa,
Uongozi si bahati, ni kadiri kuikuza!

Yarabi nipe nasaha, kusoma za kwangu dua,
Kuomba kinachofaa, sio mizigo kutwaa,
Baa kuniepushia, husuda nazo hadaa,
Uongozi si ving'ora, bali ni unyenyekevu!


Januari 27,2012
Dar es salaam

No comments: