Tuesday, January 17, 2012

Tatizo kabila lako

Na watu niliambiwa, sio watu wa kushika,
Ni wanaokunyenyekea, kwenye yako madaraka,
Juu wakinyanyukia, vya chini huvinyapaa,
Tatizo si lako wewe, tatizo kabila lako.

Mbio zao za mvua, hukaribia masika,
Huwa ni za kubagua, vya kuacha na kushika,
Roho haitoangaliwa, ila unachokishika,
Tatizo si lako wewe, tatizo kabila lako.

Ni watu wa kuwatoa, sio wa kujumlika,
Mioyo hawakupewa, ila bidhaa waweka,
Viumbe wa kutumiwa, hawanayo ya kushika,
Tatizo si lako wewe, tatizo kabila lako.

Ni watu wa kuezua, wachache wa kuezeka,
Ni watu wa kuhamia, kugura bado rauka,
Viumbe wasiojua, kwao kilicho hakika,
Tatizo si lako wewe, tatizo kabila lako.

Si watu wa kuamua, vyema yanayoeleweka,
NI chui wakijivua, juu kilichofunika,
Kondoo humdhania, kumbe jibaba la paka,
Tatizo si lako wewe, tatizo kabila lako.

Si watu wa kutambua, pendo linapopandika,
Huishia ya kulea, na sio ya kuleleka,
Shinikizo huwajia, balaa nayo mizuka,
Tatizo si lako wewe, tatizo kabila lako.

Ni watu wa kubabia, huiba wasiyopika,
Kisha huja kupakua, wajidai wamepika,
Ni chombo cha kutumia, yakiisha huvunjika,
Tatizo si lako wewe, tatizo kabila lako.

Asante kunifungua, macho yaliyofungika,
Nililchodhania chang'aa, kumbe jaa lakunuka,
Shukrani kwepushiwa, wala sintosikitika,
Tatizo si lako wewe, tatizo kabila lako.

No comments: