Thursday, January 12, 2012

Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

Wanauchumi tanzia, nchi hii wamekua,
Kila wanachotuambia, uongo kimeumbiwa,
Nchi kuendelea, watu nao hujaliwa,
Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

Maneno yao murua, chawa kichwani yatoa,
Ila nafuu haijawa, na kuja twaihofia,
Sasa kinachotokea, kila siku kupungukiwa,
Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

Kila siku ikitua, bei huzuka mpya,
Jana ukiyanunua, kwa kumi kugharamia,
Leo ishirini yawa, kama sio kuzidia,
Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

Na wasomi watwambia, mavuno wanangojea,
Kulima bila mbolea, na kwnza mwisho kuwa,
Siachi staajabia, weledi waliokua,
Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

Ni hii Tanzania, tunayoiongelea,
Chakula kuinyanyua, na bei zikapungua,
Hadaa iliyokua, au kisomo kuvia ?
Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

Gavana keshaishiwa, nasibu aingojea,
Shibe ni mwana malevya, hawezi kujitambua,
Hakuna kilo kipya, twaweza kukisikia,
Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

Nani wa kumtegemea, bei kutokutusumbua,
Wasomi wanafulia, na wajuzi ni majuha,
Nchi inaelemewa, mzigo yashindwa tua,
Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

Malenga ninayajua, ila ninawaangalia,
Neema mlojaliwa, na akili za kujifua,
Taka hamtaziondoa, baraka hamjapewa,
Ni mfumuko wa bei, au mpasuko wa bei !

No comments: