Tuesday, January 17, 2012

Pendo ni mwili na roho

KAMA hili hujajua, macho ninakufungua,
Pendo kulikhudumia, likazidi kuchanua,
Mizani kuitumia, ni jambo linalofaa,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

Pendo la mwili likiwa, hufa mwilii ukipoa,
Au ukija lemaa, mwenzio hukukimbia,
Na mzee unapokuwa, hukurithi Changudoa,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

Roho isiporidhia, sudusi vigumu kua,
Huwa wenzi wana ndoa, au ni wenye ubia,
Hili, lile wachangia, siku zikajipitia,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

Tendo mkijifanzia, uchafu mnautoa,
Ila roho ikiwia, ni ibada yatambua,
Muumba huwajalia, mpate cha kujivunia,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

Roho na mwili vikiwa, kitu kimoja mnakuwa,
Ukicheka hatolia, ukiumwa huugua,
Raha yake yako huwa, upendacho hukijua,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

Pendo hili huwa ua, waridi la kuchanua,
Kila siku hunukia, kunyauka kutojua,
Na rangize hubakia, kama lilivyozaliwa,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

Ni libasi huivaa, mme, mke walokuwa,
Nayo huishikilia, hadi kuaga dunia,
Na wengine hukataa, mwingine kujamjua,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

Pendo huwa maridhia, mizani ikitulia,
Roho na mwili vikawa, vitu vilivyo sawia,
Kilele hukifikia, wengi wasiokijua,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

Nistahi Ewe Tawba, watu unayewaongoa,
Dhalili niliyekuwa, amani ndani kujaa,
Na kizazi kufatia, kinachokutegemea,
Pendo ni mwili na roho, vingine huwa pungufu !

No comments: