Thursday, January 12, 2012

KUNILIPA HAMUWEZI

Atayenilipa Mola, kunilipa hauwezi,
Wanangu Lila na Fila, wapo wengine wazazi,
Mkiwatendea fadhila, mtanienzi mzazi,
Kunilipa hamuwezi, atayenilipa Mola!

Ninaomba Inshallah,muwe ni bora watenzi,
Kufanya yaso madhila, kwa wapitaji na wakazi,
Na kutoabudu hela, utu ukawa ajizi,
Kunilipa hamuwezi, atayenilipa Mola!

Kwa ibada nazo sala, siwezi deni kuridhi,
Dua na toba inshallah, ni hedaya nitaenzi,
Na kujali zetu mila, badala yao washenzi,
Kunilipa hamuwezi, atayenilipa Mola!

Kwenu nikawa mbolea, iIkiniweka ardhi,
Kama ninavyowalea, wengine mje hifadhi,
Ni vyema kutumikia, kuliko kupata enzi,
Kunilipa hamuwezi, atayenilipa Mola!

Na mkiiona dola, yageuka ni ya wizi,
Muombeni wenu Mola, ayalete mageuzi,
Msije kufanza hila, mkazaa mapinduzi,

Msije kufanza hila, mkazaa mapinduzi,
Huzuka vibarakala, wakawa wakubwa wezi,
Wakaihujumu dola, kwa unyama na ushenzi,
Kunilipa hamuwezi, atayenilipa Mola!

Utandawazi aula, nchi nyingi ni makazi,
Ukizuka ukabila, iondoeni mizizi,
Muende kwenye jamala, subira na maongozi,
Kunilipa hamuwezi, atayenilipa Mola!

Muende kwenye jamala, subira na maongozi,
Atakapopenda Mola, yawabebe maamuzi,
Hata likiwa ghafala, asemalo kulienzi,
Kunilipa hamuwezi, atayenilipa Mola!

No comments: