Thursday, January 12, 2012

Ukubwa huachiwa,

Asiye na manufaa, kitu gani hukufaa,
Nafsi iliyemjaa, kitu atakusaidia?
Haya aliyetolewa, aibu anaijua?
Ukubwa huachiwa, ukiwa na manufaa.

Manufaa alovia, ni mzigo mwachukua,
Taasisi yazidiwa, kufa inatarajiwa,
Nyie mnaendelea, maiti kumchukua?
Ukubwa huachiwa, ukiwa na manufaa.

Kata inadidimia, na mfu mwaiachia?
Wasambaratika mtaa, marehemu mwachelea,
Tarafa yahujumiwa, hayati mwamwachia,
Ukubwa huachiwa, ukiwa na manufaa.

JImbo lachakachuliwa, zezeta mwamuachia?
Wilaya inapotea, na nyie mwafatilia?
Nani mnategemea, kuja kuwasaidia?
Ukubwa huachiwa, ukiwa na manufaa.

Mkoa ungelikuwa, pande lajitegemea,
Waziri mkuu akawa, mambo anasimamia,
Huku anasaidiwa, na mawaziri mkoa,
Ukubwa huachiwa, ukiwa na manufaa.

Haya yasingetokea, na uchumi ungekuwa,
Mtumba tusingevaa, mpya tingevalia,
Upele kuufagia, na chawa wa kizungu pia,
Ukubwa huachiwa, ukiwa na manufaa.

Nchi imapobagua, wengi waliobakia,
Wachache kuwatumia, ujuzi wasiokuwa,
Ndipo yamapoanzia, yale ya kule Tunisia,
Ukubwa huachiwa, ukiwa na manufaa.

No comments: