Thursday, January 12, 2012

Urijali ukiisha

Haya ninayokupasha, ya kwangu mshawasha,
Muda haraka waisha, usipoteze maisha,
Kwa bora kujishughulisha, na roho kustawisha,
Urijali ukiisha, muda nao unaisha !

Ujana unajikosha, mambo yake ya kutisha,
Anasa huzizidisha, ikawa ndiyo motisha,
Muumba wakamshusha, naye kujisahaulisha,
Urijali ukiisha, muda nao unaisha !

Ninakupa hili kasha, mwanangu sasa yatosha,
Huna la kukuchelewesha, kayaanze maisha,
Bila kitu kukishusha, ukavishika maisha,
Urijali ukiisha, muda nao unaisha !

Kwanza utaniangusha, Mola nyuma kumshusha,
Kumtanguliza maisha, hilo ninakuharakisha,
Ibadaye kukuchosha, kamwe hayo si maisha,
Urijali ukiisha, muda nao unaisha !

Urijali hutosiha, peponi uzidi tisha,
Urulaini wakosha, achana na mikengesha,
Mola akishakuvusha, hustarehe maisha,
Urijali ukiisha, muda nao unaisha !

No comments: