Saturday, January 14, 2012

Kitu gani watufaa ?

Labda stima kupaa, na bei juu kuwa,
Kisha na kila bidhaa, ghali sana kununua,
Watu wenda wakilia, nani wa kuwasikiya ?
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Ajabu wanaotembea, mengi wakajionea,
Hawana wanalotwaa, japo ikawa sanaa,
Waje kuliigizia, nyumbani wakirejea,
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Machoni tukiyatia, twaweza igilizia,
Na sisi kujiundia, chetu kitakachotufaa,
Hurudi tena kimya, mabegi yao yajaa,
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Hebu sasa angalia, Keko wanapoingia,
Mjasiriamali raia, waendapo kumvaa,
Mizani kajiundia, wao wamezikataa,
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Sasa wamshtakia, viwango havijafaa,
Ndani kumsukumia, badala kumsaidia,
Huo sio ukichaa, watu tunaokataa?
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Hawayajui Korea, zamani yaliyotokea,
Trekta kujiundia, rivasi gia zikawa,
Ila walishangilia, kwa yao kujiundia,
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Kuvumbua si kukaa, ofisini kupepewa,
Viyoyozi mwatumia, kurepea mwaishiwa,
Hii ya kwenu tabia, nawaambia ni balaa,
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Rushwa huwa wachukua, maofisa walokua,
Matajiri kuachiwa, nje wakaagizia,
Na uvumbuzi kuua, wa nyumbani ukichipua,
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Yetu tusipotumia, hata kasoro zikiwa,
Tubaki twakimbilia, nje vinvyotokea,
Mbali hatutafikia, njiani tutaishia,
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

Viongozi twaambia, watalii walokuwa,
Basi hapa mkirejea, njooni na ya kujiundia,
Vinginevyo mtakua, mwaiua Tanzania!
Kitu gani watufaa, viongozi watalii?

No comments: