Thursday, January 12, 2012

Akiongoza jogoo

NI YAKE YOTE makoo, akiongoza jogoo,
Weye hauna chaguo, ila kwayo upewayo,
Haya ni yake mazao, kutumia atakayo
Akiongoza jogoo, ni yake yote makoo.

Hana nasaba na koo, kwa yahusuyo makoo,
Na hawa na wale nao, huwa ni zake teuo,
Na wana sio mafao, mayai waenguao,
Akiongoza jogoo, ni yake yote makoo.

Hakitazami kioo, furaha yake miayo,
Kuwika akuikao, huyatafuta makoo,
Na haki asimamiayo, nayo huwahusu hao,
Akiongoza jogoo, ni yake yote makoo.

Husemwa ni ngoma droo, kwa wote wamtambuao,
Hupita vilango vyao, akahama hata kwao,
Ukubwa aupatao, hata kuwa juu yao,
Akiongoza jogoo, ni yake yote makoo.

Hayajui malimao, ya mti aupandao,
Daima lake shangao, ni makoo wapitao,
Hana lingine tambuo, ila manii mazao,
Akiongoza jogoo, ni yake yote makoo.

Huu wake mchepuo, na namba si apatayo,
Ila anao mgao, wake pia wa ukoo,
Na haki waitoayo, mkumbukeni jogoo,
Akiongoza jogoo, ni yake yote makoo.

Hili haramu pumbao, lamtawala jogoo,
Hayawani nao wao, ndiyo sasa watakayo,
Na mtu ayatakayo, ndiyo nayo apewayo,
Akiongoza jogoo, ni yake yote makoo.

No comments: