Friday, January 13, 2012

Kama Mola niko naye

Nitamwogopa mtu gani, kama Mola yuko nami,
Nani ni mwenye mizani, awezaye kunihami,
Nani ni mwenye hisani, asiye nao umimi?
Kama Mola niko naye, ni nani nitamwogopa?

Huyu siye tu Manani, bali ni wa kwangu Ami,
Nikiwepo duniani, wa kwanza kwenye ulimi,
Naomba yake auni, kuchunga wangu usemi,
Kama Mola niko naye, ni nani nitamwogopa?

Na kama nikiwa mgeni, Uturuki na Ajemi,
Naomba yake ihsani, aniepushe na watemi,
Nuru iwepo mbeleni, na nyuma ikinihami,
Kama Mola niko naye, ni nani nitamwogopa?

Nuru iwepo usoni, kuiepuka jahimi,
Kadhalika na machoni, uoni uwe wa lami,
Naye bila kusaini, iwe kitu sikifumi,
Kama Mola niko naye, ni nani nitamwogopa?

Nikuze yangu imani, katika hii jamii,
Upole na umakini, ujaze wangu ulimi,
Katika feli na kani, pasiwe kitu sipimi,
Kama Mola niko naye, ni nani nitamwogopa?

No comments: