Friday, January 13, 2012

Afrika Kwacha !!!

Kumekucha Afrika, yaanza kuendelea,
Wazungu kwao watimka, ajira kukimbilia,
Nchi zaweza jengeka, akili tukitumia,
Kumekucha Afrika, milango ifungueni!

Viongozi Afrika, watakiwa kulijua,
Waache kubabaika, maamuzi kuamua,
Kwenda hadi Amerika, vibarua kuchukua,
Kumekucha Afrika, Tanzania mnalala ?

Ulaya wanateseka, kwa ajira sio njaa,
Watu wanaweweseka, akili kutozitumia,
Na kubwa wanalolitaka, wapate kuajiriwa,
Kumekucha Afrika, milango bado mwafunga ?

Rasilimali twataka, za watu zilizokua,
Mali asili hakika, haya tulishajaliwa,
Hivi vikiunganika, Afrika itapaa,
Kumekucha Afrika, milango ifungueni!

Matatizo kuyasaka, watu yanayosumbua,
Kisha idara kuweka, elimu-kazi kuzaa,
Na iwe kuelimika, ni tatizo kutatua,
Kumekucha Afrika, Tanzania mnalala ?

Vijana wasoajirika, sasa watatamanika,
Kesho yetu kugeuka, ikawa ni ya hakika,
Majogoo wakawika, watokao Afrika,
Kumekucha Afrika, milango bado mwafunga ?

No comments: