Sunday, January 29, 2012

Cheo kilicho aali

Cheo na mtu kupewa, huweza kukiondoa,
Ila kwa wanaopewa, na umma uloridhia,
Uongozi huutwaa, nao wakamjazia,
Cheo kilicho aali, wananchi wanachokupa!

Cha mtu sijalilia, chenu ninakingojea,
Daraja kunipatia, na hadhi kunigaia,
Kwa ninayowaambia, na macho kuwafungua,
Cheo kilicho aali, wananchi wanachokupa!

Ukweli wanaojua, vipofu wameshakuwa,
Ubaya wanidhania, kwa mazuri kuwazia,
Shetani kawaiangia, yawasumbua dunia,
Cheo kilicho aali, wananchi wanachokupa!

Wa kwao wawaibia, vipi nitaangalia,
Makosa washindilia, na nchi inapotea,
Ubaya wameanzia, mimi ninamalizia,
Cheo kilicho aali, wananchi wanachokupa!

Nafsi naikataa, ya kwenu nimechukua,
Sina hata kitambaa, na mtu nilichopewa,
Kikoi ninakivaa, hadimu nimeshakua,
Cheo kilicho aali, wananchi wanachokupa!

Wanizika napumua, na wala sijawalilia,
Ni nyie nawangojea, niliowakusudia,
Msiache nifukua, walipshanifukia,
Cheo kilicho aali, wananchi wanachokupa!

Kwa sasa naazimia, ukimya kutangazia,
Nchi kuiangalia, njia inayochukua,
Mema wanaonitakia, nukuu watatumia,
Cheo kilicho aali, wananchi wanachokupa!

Dua ninawasomea, walo wema kujaliwa,
Na wabaya wakapewa, wanayoyastahilia,
Na siku ikifikia, mizani wataijua,
Cheo kilicho aali, wananchi wanachokupa!

Januari 29, 2012
Dar es Salaam

No comments: