Thursday, January 12, 2012

Mdomo kisa cha adha

Mdomo ukiachia, vita waweza kuzua,
Kuudhibiti murua, kila upigayo hatua,
Salama viungo kuwa, mwilini vilivyokua,
Mdomo kisa cha adha, na huponzwa na ulimi.

Kudhibiti inafaa, kauli tunazotoa,
Watu wanazo hisia, tofauti zilizokua,
Vinginevyo huelewa, kile unachowaambia,
Mdomo kisa cha adha, na huponzwa na ulimi.

Dua ukiitumia, huwa zinasadia,
Ukiamka kunuia, mdomo kuuzuia,
Na ulimi ukajua, yale yasiyotakiwa,
Mdomo kisa cha adha, na huponzwa na ulimi.

Mtu mchache ukiwa, wa maneno kuongea,
Usemalo kupimia, na mahala kutambua,
Makundi yaliyokuwa, ishara kuzitambua,
Mdomo kisa cha adha, na huponzwa na ulimi.

Kalima utatumia, mahala inayofaa,
Na hautosingiziwa, uongo lililokuwa,
Amani ukaijua, na hofu kuiondoa,
Mdomo kisa cha adha, na huponzwa na ulimi.

No comments: