Thursday, January 12, 2012

Vijiji pasi umeme, ni nani alaumiwe?

Ni wagumba kufikiri, mimi ninavyojionea,
Watu wataka zikiri, mkekani wamekaa,
Hata walio sifuri, hawawezi kuelewa,
Vijiji pasi umeme, ni nani alaumiwe?

Ovataimu KAFIRI, shirika linaziua,
Hakuna wa kufikii, bei zazidi kupaa,
Itayoyoma hiari, watu wakifikiria,
Vijiji pasi umeme, ni nani alaumiwe?

Ukiritimba shari, na siasa balaa,
Hakuna kilicho kheri, maafa tunangojea,
Kiongezeni kiburi, kiama chakaribia,
Vijiji pasi umeme, ni nani alaumiwe?

Nchi haina jasiri, mamluki tumekua,
Twatumiwa na kafiri, wao wazidi kupaa,
Na yetu yenye kheri, tunazdii kuambaa,
Vijiji pasi umeme, ni nani alaumiwe?

Kiumbe ungefikiri, umeme kujaenea,
Nchi ingeshamiri, na vijiji vikang'aa,
Wangezuka matajiri, vijijini kwenda kaa,
Vijiji pasi umeme, ni nani alaumiwe?

Ungepondwa ufakiri, nchi yote kupotea,
Na wanaojiajiri, miujiza wangezua,
Nchi ikawa tajiri, maskini Tanznaia,
Vijiji pasi umeme, ni nani alaumiwe?

No comments: