Thursday, January 12, 2012

Chongo huona kizima

Jicho moja nalo pia, huona kitu kizima,
Si nusu kushuhudia, ni yake kweli kalima,
Nuru yake kubwa hua, kwa vitu anavyosoma,
Chongo huona kizima, na wala haoni nusu!

Huwezi kumbagua, na yeye mtu mzima,
Huona usiyojua, kamwongezea Karima,
Hisia zake ulua, huichelea nakama,
Chongo huona kizima, na wala haoni nusu!

Ila huwa chaugua, kipofu kikiwa chama,
Nusu huyaangalia, mengine yakasimama,
Kipofu kinapokuwa, hakuna tena uzima,
Chongo huona kizima, na wala haoni nusu!

Upofu unatokea, chama kisicho heshima,
Pale kisipotambua, watu wanakitazama,
Maovu kujifanzia, hatana kubwa dhuluma,
Chongo huona kizima, na wala haoni nusu!

Watu hukichungua, wakakiona hasama,
Kisha watakichukia, na wake wenye heshima,
Chenyewe kikabakia, kisiweze kusimama,
Chongo huona kizima, na wala haoni nusu!

Dhana nimeichambua, na neno sikuazima,
Yumkini nadharia, yajua dunia nzima,
Ni wanaochipukia, wanairudisha nyuma,
Chongo huona kizima, na wala haoni nusu!

No comments: