Saturday, January 21, 2012

Daktari na mbunge, nani alipwe zaidi?

Kati yao watu hawa, nani haki itakuwa,
Mshahara kuchukua, mwingi uliotoshea,
Asiwe kupungukiwa, huduma bora kutoa?
Daktari na mbunge, nani alipwe zaidi?

Kisomo alichosomea, kwanza hebu fikiria,
Na kazi aliyopewa, muhimu ilivyokuwa,
Na muda anaokaa, watu kushughulikia,
Daktari na mbunge, nani alipwe zaidi?

Na maisha kuokoa, watu hai kubakia,
Hali wanaoumia, upya kuwatengenea,
Na afya kuangalia, siha wakajipatia,
Daktari na mbunge, nani alipwe zaidi?

Elimu wanaotoa, ubunge ukajapewa,
Maarifa wanaogawa, ujanja ukajaliwa,
Macho wanaokufungua, ukweli ukatambua,
Daktari na mbunge, nani alipwe zaidi?

Uchafu wanaotwaa, na usafi kukutia,
Choo wanaochukua, na mkojo kuwavaa,
Kusinzia wasiojua, na kulala kwa kubabia,
Daktari na mbunge, nani alipwe zaidi?

Njia wasojipatia, vingine kujichumia,
Teni pasenti wasopewa, wala rushwa kugaiwa,
Mtaji wasiokuwa, jasiriamali wakawa,
Daktari na mbunge, nani alipwe zaidi?

Nchi wasiojilia, ila wao wanaliwa,
Ukubwa wasiotumia, wengine kunyanyapaa,
Juu wanaowafaa, na chini kusaidia,
Daktari na mbunge, nani alipwe zaidi?

No comments: