Thursday, January 12, 2012

Michezo tumefulia

Michezo tumefulia, kila mtu anajua,
Redio zimebakia, wachezaji maridhawa,
Kisha wanafuatiwa, na magazeti bidhaa,
Michezo fumefulia, na huu ndio ukweli!

Soka tumeshupalia, mingine twaipindua,
Akili moja tunakua, mengi kutosaidia,
Na tuliposhikilia, panazidi kuvia,
Michezo fumefulia, na huu ndio ukweli!

Shule hatujatambua, lazima kuanzishia,
Msingi kuunyanyua, mengine yatafatia,
Sifa tunatarajia, haraka tu kusifiwa,
Michezo fumefulia, na huu ndio ukweli!

Waandishi wazidiwa, uzalendo kuutia,
Magazeti wadhania, viwanja vimeshakua,
Na redio kuingia, namba wameshagaiwa,
Michezo fumefulia, na huu ndio ukweli!

Watangazaji balaa, namba wanazichukua,
Bila uwanjani kua, wanacheza kuzidia,
Na magoli huingia, kwa mdomo kusifia,
Michezo fumefulia, na huu ndio ukweli!

Programu yatakiwa, michezo si kutania,
Na mipango ya kufaa, viwanja kujijengea,
Na vifaa kununua, wachezaji kutumia,
Michezo fumefulia, na huu ndio ukweli!

Na shule kuziridhia, baadhi ya kata zikawa,
Michezo kujivunia, umaalum kupewa,
Wote waliojaliwa, waje hapa kuja kua,
Michezo fumefulia, na huu ndio ukweli!

No comments: