Thursday, January 12, 2012

Tongotongo zikijaa

HADITHINI twaambiwa, wapo walojilambia,
Tongotongo kuzitoa, ikawa ni majaliwa,
Vibibi wakawafaa, mali nyingi kujaliwa,
Tongotongo zikijaa, macho huwa hayaoni!

Na hawa tunaopewa, tongotongo walojaa,
Nani kuwahudumia, waweze kuziondoa,
Macho kuyafungua, ukweli wakaujua?
Tongotongo zikijaa, macho huwa hayaoni!

Upofu wawatishia, washindwa kuangalia,
Na wasiposaidiwa, shimoni wataingia,
Haraka inatakiwa, tongotongo kuondoa,
Tongotongo zikijaa, macho huwa hayaoni!

Nzi wawakimbilia, kila siku wanajaa,
Ni hatari nakwambia, kinachoweza kutokea,
Uoni ukiondoa, ukubwa huwa ni jaa,
Tongotongo zikijaa, macho huwa hayaoni!

Nyikani najiimbia, hawanitaki adawa,
Ukweli kuufichua, nongwa kwao imekuwa,
Ila wapaswa kujua, sintobadili tabia,
Tongotongo zikijaa, macho huwa hayaoni!

Ni wao inafaa, utu kuurejelea,
Udhalimu kukataa, na dhulumati kutokua,
Hii ibada na dua, vingine mnajihadaa,
Tongotongo zikijaa, macho huwa hayaoni!

No comments: