Thursday, January 12, 2012

Tamaa mama wa baa

TAMAA mwanaizaya, kupendwa asiyejua,
Wengi kilio hutia, na majuto kuingia,
Ukiweza mkimbia, kimbia ninakwambia,
Tamaa mama wa baa, mikosi pia balaa!

Huyu ni mama wa baa, majanga amezoea,
Mwepesi kupakimbia, neema ilipokua,
Dhiki akaziendea, moja kwa moja kuhamia,
Tamaa mama wa baa, mikosi pia balaa!

Mikosi huinuia, kipimo kujipimia,
Debe kujimiminia, lita akaikataa,
Huba kujilimbikia, vigumu kumpungua,
Si wa kuangalia, Mola akamhofia,
Tamaa mama wa baa, mikosi pia balaa!

Salaye mali kukua, hata haramu ikiwa,
Hutaka mbele kukaa, kila anapotokea,
Mtaka kutangulia, nyuma hakukuzoea,
Tamaa mama wa baa, mikosi pia balaa!

Mikosi humsisimua, hupenda kuikaribia,
Dhuluma huziandaa, wanyonge kuwaonea,
Wajane huwahadaa, na yatima kuibia,
Tamaa mama wa baa, mikosi pia balaa!

Na kiongozi akiwa, huishi kwazo hadaa,
Huishi kwa kusifiwa, japo mengi aezua,
Nafsi humkomaa, kaburi akatania,
Tamaa mama wa baa, mikosi pia balaa!

Huzungukwa na kinyaa, marashi akadhania,
Malaika hukimbia, sehemu anazokaa,
Ibilisi pacha huwa, kila anapoingia,
Tamaa mama wa baa, mikosi pia balaa!

Tunakuswihi jamia, ibilisi kumwondoa,
Kila tunachoamua, pasiwepo na tamaa,
Wala yetu kuyatia, ya haramu manufaa,
Tamaa mama wa baa, mikosi pia balaa!

No comments: