Thursday, January 12, 2012

Michezo kama ajira

OLYMIPIKI nawaza, yaenda kutuumbua,
Hivi kweli tumeweza, michezo kuitanzua,
Au twamwomba pweza, aende kutusaidia?
Michezo kama ajira, hivi nalo tumeweza ?

Hakuna tunachoweza, hivi leo twatambua,
Kila mahala pana giza, mwanga umeshapoea,
Utafikiri tumechezwa, ngomani tulipokua,
Michezo kama ajira, hivi nalo tumeweza ?

Itokee miujiza, ndio tutafanikiwa,
Jirani watatuburuza, majuu tukiingia,
Waone twaenda cheza, si medali kuchukua,
Michezo kama ajira, hivi nalo tumeweza ?

Na neema twafukuza, kwa utani kutania,
Kujipanga tumekwaza, nje tunakimbilia,
Limeshaoza Baraza, hata jengo latitia,
Michezo kama ajira, hivi nalo tumeweza ?

Michezo tumepuuza, siasa zatusumbua,
Wenyewe tunajiuza, wajanja tunadhania,
Inafaa kupuuzwa, na kuchekwa na dunia,
Michezo kama ajira, hivi nalo tumeweza ?

Manamba tunawakweza, majukumu kuchukua,
Hivi kweli tutaweza, au ndio twapotea,
Ajizi mama wa adha, na ndivyo inavyokua,
Michezo kama ajira, hivi nalo tumeweza ?

No comments: